Tuesday, September 6, 2011

viongozi wauza madawa ya ulevya


Makongoro Oging' na Issa Mnally
Sakata la baadhi ya viongozi wa dini kuhusishwa na biashara ya madawa ya kulevya ‘unga’, sasa limeleta balaa kiasi cha maaskofu, mashehe, wachungaji na viongozi wengine wakiwemo waliopo serikalini na wafanyabiashara…

Makongoro Oging' na Issa Mnally
Sakata la baadhi ya viongozi wa dini kuhusishwa na biashara ya madawa ya kulevya ‘unga’, sasa limeleta balaa kiasi cha maaskofu, mashehe, wachungaji na viongozi wengine wakiwemo waliopo serikalini na wafanyabiashara wakubwa kutajana kwenye vyombo vya dola.


Kutokana na viongozi hao wa dini wanaouza unga kuanza kutajana, ni wazi kuwa hatapona mtu katika fagio la sasa la kikosi cha kupambana na madawa ya kulevya cha Jeshi la Polisi Tanzania.

MAJINA 500 YAPO MEZANI
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na Kamanda wa Kikosi Kazi cha Kudhibiti Madawa ya Kulevya Nchini, Godfrey Nzowa, kuna majina zaidi ya 500 ya watu waliotajwa kujihusisha na biashara hiyo haramu ambapo baadhi yao wameshakamatwa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Nzowa, watu hao wanapelelezwa na ushahidi utakapopatikana watafikishwa katika vyombo vya sheria na kuahidi kwamba kipindi hiki haponi mtu anayejihusisha na biashara hiyo.

“Kwa sasa majina ya maaskofu, mashehe au maalhaji wanaotuhumiwa siwezi kuyaweka hadharani kwa sababu watashtuka. Tunaendesha  zoezi hili kimya kimya, tukishawakamata wengine tutatangaza,” alisema Nzowa.

ZANZIBAR NA NIGERIA
Kamanda Nzowa alisema, hali mbaya zaidi ya biashara hiyo ipo katika maeneo ya Zanzibar na Nigeria ambako kunaonesha ni njia ya kupitisha madawa na baadhi ya waliokamatwa wanatoka sehemu hizo.

“Tunawachunguza viongozi wa kidini wanaopenda kwenda nchini Nigeria mara kwa mara ambao majina yao tunayo hapa katika orodha yetu. Watu hao ni watuhumiwa wa biashara hiyo. Hatutamuonea aibu mtu yeyote hata kama ana cheo kikubwa.

“Lengo letu ni kutokomeza biashara hii haramu, hawa watu ni wajanja ukimkamata mmoja aliyetumia njia fulani, kesho wanaiacha na kubuni mbinu nyingine, lakini ukweli ni kwamba tutawakamata wote,” alisema Nzowa.

BADO NI VITA YA MAASKOFU NA JK
Juni 5, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete akiwa mkoani Ruvuma alipoalikwa kwenye shughuli ya kusimikwa Uaskofu wa Jimbo Kuu la Mbinga, John Ndimbo wa Kanisa Katoliki, alisema kuna baadhi ya viongozi wa dini wanaojihusisha na madawa ya kulevya na kuwataka waache.

Kauli hiyo iliwafanya viongozi mbalimbali wa dini kumuomba kiongozi huyo wa nchi awataje hadharani kwa vile siyo watu wazuri katika jamii.
Baadhi ya viongozi wa dini ambao walikemea kitendo hicho na kumtaka Kikwete awataje hadharani ndani ya saa 48 ni wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania inayoongozwa na Askofu Peter Kitula akisaidiwa Dk. Valentino Mokiwa.

Baadhi ya maaskofu wa jumuiya hiyo ni Alex Malasusa, Godfrey Mdimi, Alinikisa Cheyo, Thomas Laizer, Stanley Hatay, Marterus Kapinga na  Oscar Mnunga.

Aidha, Baraza la Maaskofu Tanzania ambalo mmoja wa viongozi wake ni Kadinali Polycarp Pengo lilikuja juu kutokana na Kikwete kutolea kauli hiyo katika hafla ya kumsimika askofu wao, wakidai kuwa wanaweza kueleweka vibaya kwa waumini wao, hivyo kumtaka rais kuwaanika wahusika.

Baadhi ya maaskofu wa Katoliki wanaoongozwa na baraza hilo ni Anthony Petro, Jude  Ruwaichi na Method Kilaini.

Viongozi wa makanisa ya kiroho pia walitaka kuwajua waliohusika na biashara hiyo haramu kwa madai kuwa ni kinyume na maadili ya dini yao, hao ni pamoja na Askofu Zachary Kakobe, Askofu Sylivester Gamanywa ambaye alisema tamko la Kikwete ni bomu lililolipuka katika kambi ya dini.

Kwa upande wa Waislamu, Mufti Issa Shabani Simba naye alipinga viongozi wa dini kujiingiza katika biashara hiyo haramu na kuitaka serikali kuwashughulikia watu hao.

MAONI YA VIONGOZI WA DINI
Gazeti hili wiki iliyopita lilifanya mahojiano na baadhi ya viongozi wa dini kuhusiana na mtazamo wao juu ya madawa ya kulevya ambapo walikuwa na haya ya kusema:

Askofu Dk. Mwambigija Eric wa Kanisa la Church of God of Prophecy lililopo Liwiti Tabata alisema, madawa ya kulevya ni dhambi hivyo kwa kila hali ni lazima suala hili lishughulikiwe kiroho.

Imamu wa Msikiti wa Manyema, Kariakoo, Abubakar Hussen alisema: “Kikwete ni kiongozi wa nchi, hivyo ana uwezo wa kuonya kama kuna jambo baya na viongozi wa dini ni kioo cha jamii, sasa  kama kuna wanaofanya  biashara hiyo haramu wajisafishe  ili wawe mfano bora.

Askofu Chesa Elias wa Victorious Church of Tanzania alisema: “Vijana  wakikataa  kutumiwa na  kuamua kujiunga  na  vikundi vya ujasiriamali biashara hii itakufa,  sisi huku  kanisani  tumeanzisha  mafunzo  kwa watu mbalimbali  wakiwemo  vijana  ili wawe na ujuzi  baadaye  wapate  mkopo.”

Sheikh Adam Omar wa Tandale alilaani kitendo cha watu wa aina zote kujihusisha katika biashara hiyo kwani tayari vijana wengi wameharibika.
Naye Askofu John Said  wa Kanisa  la Victorious, Mabibo External, Dar alisema: “Rais Kikwete kama kiongozi wa nchi ana nafasi ya kukemea maovu, nasi viongozi wa dini tunatakiwa kumsaidia ili  kama wapo wale walioingia katika dini kwa lengo la biashara hiyo haramu, waache kabisa."

Naye Mchungaji Atilio Komba wa Kanisa la Habari Njema lililopo Mbezi jijini alisema kuwa analaani viongozi wa dini wote ambao wanajihusisha na mihadharati.  
 
Mwinjilisti Medad Anjelo wa Kanisa la TAG Mbagala alisema, biashara ya madawa ya kulevya ni tatizo kubwa la kitaifa na serikali inastahili lawama kwa sababu vijana waathirika wapo na hawaulizwi wanaowauzia ili wabanwe. 

Mwinjilisti Zebedayo Mwangunda  wa Full Salvation Church la Mikocheni “B” alieleza kuwa ana shaka na utendaji wa serikali kuhusu sakata la madawa ya kulevya.

KIRUNGU CHA JK
Wiki iliyopita wakati akihutubia Baraza la Idd, JK alisema, watumishi wa Mungu wanaouza madawa ya kulevya ni wengi na vitendo wanavyofanya ni hatari ndiyo maana hata wabunge walilia walipooneshwa mkanda wa video.

Alisema, wapo maaskofu, mashehe na maalhaji, kwa hiyo aliwataka watu wasiingilie kazi ya serikali wanapoanza kukamatwa.

0 comments: