Tuesday, September 6, 2011

Bi. Kizee: Tangu nipigwe mabomu, nimeambulia karatasi ya chooni tu!

KARATASI za chooni (tishu) zinaweza kuwa msaada muhimu kwa mwathirika wa mabomu! Kwamba mtu abomolewe nyumba, akose makazi, yaani kulala kwake shida na mateso lakini huyo huyo anapewa tishu zimfariji.

Leo ni miezi sita na siku 23 tangu wakazi wa  Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam walipuliwe na mabomu yaliyokuwa kwenye ghala kuu la silaha za kijeshi, Kikosi namba 511 cha Jeshi la Wananchi Tanzania.

Kumbukumbu ya tukio hilo kwa bibi kizee, Mkegani Mohamed Sultan, 66, (pichani)  ni maumivu makubwa, kwani licha ya serikali kuahidi kuwasaidia waathirika wa mabomu, yeye alichoambulia ni karatasi ya chooni.

“Baada ya milipuko ya mabomu, sijawahi kupata msaada wowote  licha ya nyumba yangu kuharibika vibaya. Nina familia ya watu tisa. Niliwahi kusaidiwa na Taasisi ya Msalaba Mwekundu  karatasi za chooni pakiti mbili na baada ya hapo sijaona msaada wowote toka serikalini.”

WAATHIRIKA WENGINE KILIO
Zaina Binti Mohamed anayeishi Mtaa wa Mahita Ukonga huku akitokwa na machozi alikuwa na haya ya kusema: “Mimi baada ya nyumba yangu kubomolewa na mabomu sina pa kuishi pia huduma ya chakula sipati.

“Huwa najiuliza kwa nini serikali inatutelekeza? Hii serikali kweli inajali watu wake? Maswali hayo na mengine mengi ninapojiuliza huwa sipati jibu nabaki nalia. Unaona haya mahema niliyopewa ? Mvua yote ilikuwa yangu, yamekwisha, yametoboka.

“Maisha yangu na ya familia yangu ni ya kubahatisha, tumelala katika mahema haya mpaka yamechakaa, serikali imetusahau na imeenda kinyume na kauli yake kuwa tutahudumiwa na kupewa kila msaada. Serikali gani inasema uongo na kwenda kinyume na kauli inayowaambia wananchi wake tena wenye shida?

“Mimi nasaidiwa na Msikiti wa Gongo la Mboto lakini kuna baadhi ya watu walioathirika na mabomu nasikia wanapata misaada, huwa najiuliza wanapata kwa utaratibu gani ili nami nipate? Sipati jibu.”

Uwazi liliwafikia waathirika wengi ambao  hadi sasa wanaishi kwenye mahema mabovu yaliyotoboka kama ya wakimbizi na wengine kwenye vibanda ambavyo walijengewa na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa ambavyo sasa  vimechoka.

Wananchi hao wanadai kuwa kwa sasa hawana mahala pa kulala kutokana na vibanda hivyo  kubomoka na hawana msaada wowote kutoka ngazi ya kata hadi mkoani.

KAULI YA UONGOZI WA MTAA
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mather Care aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwaluko ambao bi mkubwa  Zaina anaishi alikiri kufahamu matatizo ya wakazi hao akasema: “ Ni kweli matatizo yao tunayatambua  lakini serikali ilitoa maelekezo kuwa kuna  watu wangepewa kipaumbele.

“Nikiri tu kuwa  ni kweli Bi Mkegani hakupata msaada kama ambavyo inastahili.” Jitihada za kumpata Mwenyekiti wa Kata ya  Gongo la Mboto hazikuzaa matunda  lakini  mmoja wa wajumbe wa serikali yake aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji alisema kuwa ni kweli  malalamiko hayo  ya waathirika yapo na wanashughulikia kwani ni jukumu lao.

KAULI YA MKUU WA WILAYA YA ILALA
Mkuu wa Wilaya Ilala, Leudanis  Gama kwa upande wake alisema kuwa serikali iko macho na suala hilo na  kuna kamati ambazo zinafuatilia kwa ukaribu zaidi na mara nyingi wamekuwa wakitembelea  waathirika hao na zoezi hilo itaendelea hadi hapo kila mmoja atakapopata sehemu sahihi ya kuishi, kula na kuvaa.

Wananchi wakazi wa Ukonga wanadai kuwa kauli ya Rais Kikwete  imepuuzwa kwani baada ya kuagiza wasaidiwe haraka  hakuna kilichotekelezwa na ni aibu kwa dola.

0 comments: