KARATASI za chooni (tishu) zinaweza kuwa msaada muhimu kwa mwathirika wa mabomu! Kwamba mtu abomolewe nyumba, akose makazi, yaani kulala kwake shida na mateso lakini huyo huyo anapewa tishu zimfariji.
Leo ni miezi sita na siku 23 tangu wakazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam walipuliwe na mabomu yaliyokuwa kwenye ghala kuu la silaha za kijeshi, Kikosi namba 511 cha Jeshi la Wananchi Tanzania.
Kumbukumbu ya tukio hilo kwa bibi kizee, Mkegani Mohamed Sultan, 66, (pichani) ni maumivu makubwa, kwani licha ya serikali kuahidi kuwasaidia waathirika wa mabomu, yeye alichoambulia ni karatasi ya chooni.
“Baada ya milipuko ya mabomu, sijawahi kupata msaada wowote licha ya nyumba yangu kuharibika vibaya. Nina familia ya watu tisa. Niliwahi kusaidiwa na Taasisi ya Msalaba Mwekundu karatasi za chooni pakiti mbili na baada ya hapo sijaona msaada wowote toka serikalini.”
WAATHIRIKA WENGINE KILIO
Zaina Binti Mohamed anayeishi Mtaa wa Mahita Ukonga huku akitokwa na machozi alikuwa na haya ya kusema: “Mimi baada ya nyumba yangu kubomolewa na mabomu sina pa kuishi pia huduma ya chakula sipati.
“Huwa najiuliza kwa nini serikali inatutelekeza? Hii serikali kweli inajali watu wake? Maswali hayo na mengine mengi ninapojiuliza huwa sipati jibu nabaki nalia. Unaona haya mahema niliyopewa ? Mvua yote ilikuwa yangu, yamekwisha, yametoboka.
“Maisha yangu na ya familia yangu ni ya kubahatisha, tumelala katika mahema haya mpaka yamechakaa, serikali imetusahau na imeenda kinyume na kauli yake kuwa tutahudumiwa na kupewa kila msaada. Serikali gani inasema uongo na kwenda kinyume na kauli inayowaambia wananchi wake tena wenye shida?
“Mimi nasaidiwa na Msikiti wa Gongo la Mboto lakini kuna baadhi ya watu walioathirika na mabomu nasikia wanapata misaada, huwa najiuliza wanapata kwa utaratibu gani ili nami nipate? Sipati jibu.”
Uwazi liliwafikia waathirika wengi ambao hadi sasa wanaishi kwenye mahema mabovu yaliyotoboka kama ya wakimbizi na wengine kwenye vibanda ambavyo walijengewa na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa ambavyo sasa vimechoka.
Wananchi hao wanadai kuwa kwa sasa hawana mahala pa kulala kutokana na vibanda hivyo kubomoka na hawana msaada wowote kutoka ngazi ya kata hadi mkoani.
KAULI YA UONGOZI WA MTAA
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mather Care aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwaluko ambao bi mkubwa Zaina anaishi alikiri kufahamu matatizo ya wakazi hao akasema: “ Ni kweli matatizo yao tunayatambua lakini serikali ilitoa maelekezo kuwa kuna watu wangepewa kipaumbele.
“Nikiri tu kuwa ni kweli Bi Mkegani hakupata msaada kama ambavyo inastahili.” Jitihada za kumpata Mwenyekiti wa Kata ya Gongo la Mboto hazikuzaa matunda lakini mmoja wa wajumbe wa serikali yake aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji alisema kuwa ni kweli malalamiko hayo ya waathirika yapo na wanashughulikia kwani ni jukumu lao.
KAULI YA MKUU WA WILAYA YA ILALA
Mkuu wa Wilaya Ilala, Leudanis Gama kwa upande wake alisema kuwa serikali iko macho na suala hilo na kuna kamati ambazo zinafuatilia kwa ukaribu zaidi na mara nyingi wamekuwa wakitembelea waathirika hao na zoezi hilo itaendelea hadi hapo kila mmoja atakapopata sehemu sahihi ya kuishi, kula na kuvaa.
Wananchi wakazi wa Ukonga wanadai kuwa kauli ya Rais Kikwete imepuuzwa kwani baada ya kuagiza wasaidiwe haraka hakuna kilichotekelezwa na ni aibu kwa dola.